facebook

Monday, April 28, 2014

Uchambuzi: Fid Q – Siri Ya Mchezo!

Siri ya Mchezo ni wimbo mwingine kutoka kwenye santuri mpya ya Fid Q inayoitwa Kitaalojia. Ukisikiliza vizuri, utunzi wa wimbo huu ni kama unataka kushabihiana na ule wa “Propaganda”. Maudhui ya Siri Ya Mchezo yanagusa sehemu kuu mbili. Moja ni tasnia ya muziki, hasa huu wa kizazi kipya na pili ni ulingo wa siasa. Tasnia ya muziki inamgusa Fid Q mwenyewe moja kwa moja, ingawa si hivyo na siasa kwani yeye sio mwanasiasa. Mashairi yake lakini ni mashairi yenye uanaharakati, yaani “political consciousness”.
siri ya mchezo
Mdundo wa Siri ya Mchezo ni wa kawaida, labda kwa sababu Fid alitaka tusikilize mashairi zaidi kuliko mdundo. Kiitikio cha Juma Nature kwa mtazamo wangu kingependeza zaidi kama kingepambwa na sauti ileeeee kama ya kwenye Sonia, iliyokuwa na mahadhi kama ya kaswida kaswida hivi.
Denzel Washington wa Cry Freedom, ndiyo yule Steve Biko wa Afrika Kusini?
Kitu kinachovuta hisia zangu kwa karibu zaidi katika mstari wa kwanza ni jina la Biko. Marehemu Steve Biko alikuwa mwanaharakati wa haki za watu weusi wa Afrika ya Kusini dhidi ya utawala wa makaburu. Biko alihamasisha watu weusi kujipenda wenyewe, “black is beautiful”. Fid anaghani, “stimu zikanipa elimu ya Biko”. Elimu ambayo Fid anazungumzia ni hii ya uanaharakati, kwani Biko kitaaluma alisomea udaktari. Mashairi ya Fid nayo yanatetea haki za wanyonge dhidi ya tabaka la wanyonyaji, mfano viongozi wala rushwa na mafedhuli, au kwa jina jingine, wafadhili — wafadhili wa “ukoloni mambo leo”.
Fid haoni aibu kuweka bayana uwerevu wake wa mambo “wanapagawa na baadhi ya mambo nayoyajua”. Kwa mfano, wangapi tulimfahamu Biko kabla ya Fid kumtaja? Fid anaposema “elimu ya Biko”, mimi inanipa maana mbili tofauti. Maana ya kwanza ni mbinu alizotumia Biko kufanya uanaharakati wake. Ukifanya utafiti utagundua Biko hakufundishia darasani, bali alifanya uanaharakati kwa njia ya mihadhara tena kwa kujificha.
steve bikoSasa swali ni, je, Fid na yeye anatuelimisha na uanaharakati wake kwa njia ya nyimbo zake kama Biko alivyofanya na mihadhara yake? Elimu hiyo ya Biko ndio iliyohamasisha Kitaalojia? Inawezekana nyimbo za Fid ni zaidi ya burudani, bali ni mihadhara pia, au elimu isiyo rasmi (informal education). Falsafa ya Biko ilikinzana na elimu ya makaburu ambayo ilichochea ukandamizaji. Je, elimu yetu mashuleni inafanana na hiyo ya makaburu kwa kudumaza uwezo wa kuchanganua mambo na kufikiri, ukilinganisha na elimu iliyomo ndani ya mashairi ya Fid Q ambayo yanathubutu kutulazimisha kufikiri?
Maana ya pili ya “elimu ya Biko” kama nilivyoelewa, utagundua, pamoja Biko alisomea udaktari, lakini uanaharakati wake ulimpeleka kwenye siasa pia; “black consciousness”. Biko alikuwa mwerevu wa sheria pia, pamoja haikuwa taaluma yale, lakini alijisomea mwenyewe mpaka akawa gwiji. Hapo unaweza kuona jinsi Fid Q alivyofuata nyayo za Biko. Pamoja Fid ni msanii, lakini anajua mambo mengi kama sosholojia, siasa na mambo mengineyo kwa kujisomea tu mwenyewe.
Lakini Biko ameathiri kwa kiasi gani maisha ya Fid Q? Biko amemsukuma Fid afanye nini zaidi ya kuandika mashairi ya uanaharakati? Kwani, pamoja ya kwamba Biko aliandika hotuba kali, kama Fid na mashairi yake, Biko alikuwa mstari wa mbele kupigania haki kwa vitendo, na ndio huo ujasiri uliopelekea kuuwawa kwake na utawala wa makaburu. Ni muhimu tuelewe kuwa, kujua (awareness) ni kitu kimoja, na kutenda (to act) ni kitu kingine.
Kwenye ubeti huo huo wa kwanza, Fid Q anaturudisha kwa mwanaharakati wa hapa nyumbani. Almasi ya Bandia na kitabu cha Makuwadi wa Soko Huria, ni vitabu vilivyoandikwa na Marehemu Professa Chachage. Hapa tena, Fid anazidi kuonyesha uwezo wake wa kujua mambo kupitia upenzi wake wa kujisomea vitabu. Elimu haipo tu darasani kama wengi tunavyofikiria. Kwa upeo aliokuwa nao Fid, lazima ujiulize ni mantiki gani ilitumika na viongozi katika hoja yao iliyodai kuwa, vitabu vingi (riwaya za kufundishia fasihi) mashuleni vinachanganya wanafunzi na sio kuwaongezea maarifa.
Kitabu cha Makuwadi wa Soko Huria kinachanganua utandawazi, au kama ujulikanavyo siku hizi, utandawizi. Mawazo na nasaha za Chachage kuhusu utandawazi ni kali, hivyo ni changamoto kwako msomaji kukitafuta hicho kitabu na kujisomea mwenyewe.
makuwadi1
Katika mstari wa “zawadi ya almasi ya bandia”, mimi nilijikuta nikikumbushwa ile hadithi aliyosimulia Mwalimu Nyerere kuhusu Zuzu. Zuzu alikuwa na almasi ya kweli, kwa bahati mbaya au nzuri, alitokewa na mtu aliyekuwa na kipande cha chupa. Yule mwenye kipande cha chupa alifanikiwa kumshawishi Zuzu, mpaka Zuzu aliamini kwamba almasi yake ilikuwa almasi ya bandia, na kipande cha chupa cha yule bwana ndio almasi halisi. Masikini Zuzu alikubali kubadilishana, akiondoka na furaha akifikiri amepata kumbe yeye ndiye aliyepatikana. Unadhani hadithi hii inaakisi ukweli baina yetu sisi na wawekezaji?
Mistari ya mwisho ya ubeti ya kwanza inaanza kukupa picha ni jinsi gani kitabu cha Chachage kimemgusa Fid Q. Anaghani kwa kusema, “taifa la kondoo huendeshwa na serikali ya dubu”. Hapo lazima ushikwe na hamu ya kutaka kujua dubu ni mnyama mwenye tabia za aina gani. Matumizi ya kondoo hapa yanaweza kukufanya ufikirie Biblia, Yesu na kondoo wake. Kondoo huchungwa, na leo hii wachungaji wenyewe ndio hawa viongozi ambao wamekosa uaminifu. Wakati Yesu alichunga kondoo zake, hawa miungu watu wanatutupa kwenye vinywa vya  “mabepari” ambao hawana tofauti na “mbwa mwitu”.
Mwisho wa ubeti Fid anarudi kwenye utetezi wa vijana. Huu ukoloni mambo leo “unafanya vijana wanaumia”, Fid anaghani. Hapa inaweza kuwa ni suala zima la vijana kuzidi kukosa nafasi, kwani madhara yake yanaweza kuwa makubwa. Imam Abbas kwenye Bila Sanaa anaghani kwa kusema, “vibaka wa leo ni majambazi wa kesho”. Rick Ross pia kuna wimbo anaghani kwa kusema, “if I’m low on funds, I’m a load up guns”. Haya si maneno mepesi, hasa tukizingatia tayari kumepatikana kambi za kufundisha vijana ugaidi hapa Tanzania.
Mstari wa mwisho kabisa, anasema vijana “tunaishia kufia mabatani kama nzi ndani ya chupa ya bia”. Fid anazungumzia watu wanaokufa kwenye starehe. Hii inaweza kutokana na ukweli kuwa kwenye starehe hakukosekani mambo au vitu vya anasa. Huu utamaduni wa kupenda starehe sisi vijana ndio tumeupa kipaumbele kuliko mambo ya msingi. Taswira ya nzi katika chupa ya bia inanikumbusha wimbo wa Kendrick Lamar “Swimming Pools”.
Lakini je, inawezekana vijana tunapenda kupombeka (ulevi) kutokana na kukosa imani na maisha yetu ya baadae, hivyo misongo ndio inayotupelekea tuwe walevi?
Mara ya kwanza niliposoma mstari wa “kufia mabatani”, nilidhani ni mabatini, hivyo tafsiri yangu ya haraka haraka, nilidhani Fid Q anazungumzia kituo cha polisi cha Mabatini, Sinza. Sasa tafakari, kama vijana wengi hawana ajira (sababu moja ya misongo ya vijana), na kuzurura ni kosa kisheria, basi ukweli ni kuwa wengi tutajikuta tumelundikwa polisi Mabatini.
Lakini kinachotisha zaidi ni utekelezaji wa sheria. Fid anaposema kufia, anaweza kuwa akimaanisha hivyo hivyo, kufia Mabatini. Kuna hadithi nyingi za vijana wanakamatwa kwa kosa la kuzurura, lakini wanaishia kubambikiziwa kesi kubwa kama za mauaji, na kujikuta wakisota jela kwa miaka mingi, wakitumikia vifungo vya watu wengine. Mfumo wa sheria umeathiriwa na rushwa. Hili suala la rushwa tutaendelea kulijadili kwenye sehemu ya pili, tuone ni vipi linaunganisha tasnia ya muziki na siasa — kwani hiyo ndio inaweza kuwa ni moja ya siri zilizojificha kwenye mchezo mzima.