Wasanii wengi waliojengeka na kutengemaa wana sifa nyingi, lakini mara nyingi kila msanii ana kitu kimoja ambacho kinamweka kwenye mwanga.
JCB ni mkongwe, na kitu ambacho kinamtambulisha ni uwezo wake wa kuipa mitaa sauti. Ameegemea zaidi kwenye kuhadithia vinavyotokea kwenye mitaa yetu, huku akiongea kama mmoja wetu; wanaoishi au wale waliopitia maisha ya mitaani.

Ni heshima ya pekee kwa tovuti hii kupata fursa ya kubadilishana mawazo na JCB. Kama kawaida yake, alikuwa na mengi ya kuongelea — kuanzia jinsi alivyoingia kwenye gemu hadi mawazo yake juu ya mwelekeo wa Hip Hop Tanzania.
1. JCB ni nani hasa? Na jina lako ulilipata wapi na linamaanisha nini?
Maana ya JCB ni ‘Jesus Come Black’. Kitambo ilikuwa ‘Jesus Come Back’… mshikaji wangu Spark Doggy ndio alinipa hicho kirefu, lakini mimi nilikuwa bado najiita JCB Black; kipindi hicho kama mwaka 1993 hivi.
JCB limetokana na jina langu Jacob… ukitoa “a” na “o” unapata JCB. Na kutumia “Jesus Come Black” ni kujitambua tu kama mtu mweusi.
2. Ilikuwaje ukaingia kwenye fani ya Hip Hop? Kuna watu waliokupa muongozo au kukuvutia na ukaona na wewe ujaribu?
A-Town ni mji wa Hip Hop toka kitambo, kwa hiyo kuanzia kipindi nakua nilijikuta niko katika mazingira ya Hip Hop. Ndio maana nikavutiwa na Hip Hop. Pia, marehemu kaka yangu, Richard alikuwa ananipeleka disko nilivyokuwa mdogo sana, nilikuwa napenda kucheza break dance.
Kwenye kipindi hicho mara wakatokea watu kama Saleh Jabir, wakaanza kughani kwa Kiswahili. Kwa kweli ilinipa changamoto sana! Watu wengine walionifanya niingie kabisa kwenye Hip Hop ni kama Wagumu Weusi Asilia, Kwanza Unit, Mr II, na watu kama hao.
3. Chindo alitueleza jinsi kundi la Watengwa lilivyoanzishwa, na tungependa wewe utueleze harakati za Hip Hop Arusha. Kuna mwamko wa kipekee wa Hip Hop Arusha, hii inasababishwa na nini?
Mwamko wa Hip Hop Arusha umekuwa mkubwa sana, na ukichukulia watu kibao wanakubali Hip Hop ipo A-Town kwa sasa. Tunajivunia kwa hilo na ninadhani tunatengeneza njia nzuri kwa vizazi vijavyo, kuifanya Hip Hop kuwa ajira kabisa kwa vijana.
4. Kwa upande wa Watengwa, mmekuwa “underground” kwa muda mrefu, ila nadhani heshima mmeipata tokea mwanzoni kabisa. Kujulikana kwenu sasa hivi unadhani kutabadilisha malengo yenu kwenye gemu?
Malengo hayawezi kubadilika kwa sababu muziki iliotuweka hapa ni wa ki-undeground. Sema tunataka kuufanya utupatie maslahi kidogo na kuuboresha kuendana na muda.

5. Aina ya uandishi wako ni adimu, na haujabadilisha msimamo wako! Unawashauri nini wasanii chipukizi?
Kila mtu ana mtindo wake kiuandishi, na muziki pia unahitaji mazoezi. Kwa hiyo kila siku unapokuwa unafanya huo muziki unajikuta unazidi kuboresha mtindo wako. Mi’ nawambia bwana wadogo wanaokuja kwenye game wakomae tukibibwa, mambo yatakuwa poa. Sio mambo ya kuiga style hapa…
6. Hongera kwa kupata tuzo ya Kili kupitia wimbo wako “Ukisikia Paa”, kama wimbo bora wa Hip Hop, ile tuzo wewe unaichukuliaje?
Ile tuzo ilikuwa ni ya wana-Hip hop wote, hususan wa Arusha! Hapo nyuma watu walikuwa hawaamini kama mtaa unaweza kuja kuona tuzo. Kwa kweli ilileta heshima ya Arusha kinoma!
7. Vipi upande wa miradi yako binafsi, unaridhishwa na mapokezi ya albamu yako? Kuna siku ulisema umeshindwa kuelewana na MAMU ili albamu ya pili iingie sokoni. Sasa unajipangaje na mashabiki wako wategemee nini?
Albamu yangu ilipokelewa poa na raia, ila tatizo lilikuwa ni usambazaji arif. Ujue niliiuza mwenyewe mkononi kutokana na mdosi kutaka kunipa fungu dogo sana. Nikaanza kusukuma mzigo mi’ mwenyewe na wana, na tulipata faida mara saba ya mdosi. Lakini tatizo ni kuwa kuna mikoa tulishindwa kufikisha mzigo.
Nakala za Makala Vol 2 imekamilika tayari, ila ndo hivyo bado najipanga tena kuuza mwenyewe Disemba… Bado Serikali haijatutupia jicho.
8. Ukiacha muziki, umekuwa mstari wa mbele kuwasihi vijana wa Arusha kuacha fujo na kupigana/kuchomana visu (beto), hasa baada ya kupoteza mwenzenu hivi karibuni. Mapokezi ya kampeni yenu yalikuwaje?
Hiyo kampeni inaendelea na niko karibu kukutana na wasanii wenzangu wa Arusha kukaa chini na kupiga tamasha moja kabambe. Ila tunataka kuishirikisha na serikali kwa sababu hii ni ishu ya kijamii zaidi. Kabla mwaka haujaisha lazima tamasha hili lifanyike, niko kwenye mikakati za kumuona mbunge wa jimbo langu la Arusha Mjini ili kuomba mawazo yake juu ya hilo tamasha. Ila yuko busy kinoma!
9. Kwa ujumla, unaonaje muelekeo wa Hip Hop Tanzania?
Muelekeo poa sana kwa sisi wasanii wa Hip Hop, tumejaribu kuupaisha muziki huu. Tatizo ni hakuna compuni nzuri inayosimamia kazi za wasanii katika mauzo na vitu kama hivyo. Hatuna haki miliki ya ukweli, mapromota feki kila siku wanaibuka na kuwanyonya wasanii. Serekali ingetutupia jicho kidogo ingekuwa mwake sana. Sema ndio hivyo tunakomaa nao tu.
10. Tuna freestyles kadhaa za zamani tunazo… mara nyingi Hasheem Dogo, wewe, Chindo na Watengwa wengine, na hata Fid Q, walishiriki. Bado mnafanya yale mambo? Hasheem yuko wapi siku hizi?
Freestyles zipo zakutosha arif, ujue zamani tulikuwa tunapiga sana freestyles kwa sababu ilikuwa ni mazoezi ya ubongo. Kwa sasa hivi ubongo umeshajengeka vya kutosha, unakuta zile freestyles unazopiga zinakuwa nyimbo sasa.

11. Kwa kumalizia, tunaomba utupe Top 5 emcees wako kutoka Bongo!
Wa kwanza atakuwa Hasheem Dogo. Jamaa ametupa mbinu sana za kuandika na ku-freestyle. Hasheem is my B.I.G Smallz… nampa heshima kama [ya] Notorious. Wa pili, Jay Moe na Solo Thang, popote hawawezi kuchezea beatkuanzia style na flow; Wateule ni noma. Wa tatu ni Ngosha. Fid Q ni noma…nilimpigia simu niliposikia Neno. Ngosha kiboko yao. Wa nne ni Chindo, ukija katika battles Bongo, hakuna anayeweza kumpiku mwanangu Chindo. N’na-miss kinoma katika muziki huu wa sasa huku TZ. Wa tano ni Lunduno bwana, hawa machalii wataipeleka mbali sana game ya Bongo. Hasa One, namkubali kinoma…
Tunamshukuru JCB kwa kutupa nafasi ya kufanya mahojiano nasi. Tunamtakia kila la heri yeye na wasanii wote kutoka Arusha kwenye harakati zao. Pamoja, inawezekana!
No comments:
Post a Comment