Ni emcee ambaye anaheshimika. Ametoka mbali na anafikiria mbali. Wale ambao wamepata nafasi ya kumsikiliza vizuri wanajua naongelea nini.
Album yake “The Future” ni ya kipekee. Sio kwa sababu ina nyimbo kibao, bali ina nyimbo nyingi na za kutosha za maana. Anahakikisha anawasilisha kitu makini kwenye kila verse. Wimbo wa kwanza kuanza kusikika hewani kama single ulikuwa “Nakwenda”:
Kuna wimbo mwingine ambao una ladha tofauti kidogo “Tik Tak”:

Tulipata nafasi ya kumuuliza mambo mbalimbali kuhusu yeye binafsi na kundi au familia ya Watengwa, na mahojiano yalikuwa kama ifuatavyo:
1. Chindo, Umbwa Mzee, au Lutuno kutoka Utengwani au Watengwa, hebu tupe tafsiri ya majina yako kwa kifupi…
Kwanza, nashkuru sana mtu mzima kwa kunipa nafasi hii ya kipekee kuongelea suala muhimu sana maishani mwangu!
Nianze na tafsiri ya majina yangu kama ulivyouliza. Chindo ni jina la mtaa tokea mdogo wakati tukicheza michezo ya kujificha (picaboo), ambalo wenzangu kitaani walinibatiza. Umbwa Mzee ni jina la muziki… nilijiita hivyo kama wasanii wengine. Mara nyingi wanamuziki hawatumii majina yao halisi… ni mara chache sana. Lotuno ni jina la ukoo wangu. Mimi naitwa Lomayani Lotuno. Ni jina la Kimasai kwa kuwa mimi ni Mmasai asilia. Linamaana “m’batizwaji”… kidini zaidi!
2. Umeshuhudia gemu ya Hip Hop Tanzania, hasa Arusha, tokea inaanza hadi sasa hivi. Wewe umeingia kwenye gemu lini hasa na nini kilikusukuma uanze kufanya Hip Hop?
Mimi niliingia kenye game rasmi mwaka 1997 nilivyoanza masomo ya sekondari, Namanga secondary school. Kabla ya hapo nilikuwa nasikiliza sana nyimbo za kina MC Hammer, Kool Moe Dee, Busy Bee, Public Enemy, Snoop na Dre, NWA, Warren G, Salt n Pepa, Heavy D na wengine wengi.
Kaka yangu alikuwa mtu wa old skool sana, na alikuwa ananunua tapes nyingi sana na tulikuwa na santuri kibao nyumbani. Kwa kifupi tu, nilikulia katika mazingira ya Hip Hop kwa ujumla. Nakumbuka kaka alikuwa ananinyoa kama kama MC Hammer. Mi’ sikujua kinachoendelea… nilikuwa naona kaka mtu poa sana! Kadri muda ulivyokuwa unaenda ile spirit ilikuwa inajijenga damuni mdo mdo.
3. Ilikuwaje ukaingia kwenye familia kubwa ya Watengwa? Tupe undani wa familia yenu.
Familia ya Watengwa ilianzishwa mwaka 2002. Baada ya kumaliza masomo ya computer programming Aptech, niliamua kuanzisha studio ili nisihangaike kwenda Dar kurekodi, kwa kuwa kipindi hicho Arusha kulikuwa hakuna studio. Mimi na JCB tuliamua kuungana na kuanzisha chama ‘Watengwa’… kikundi na studio yake.
Kabla ya hapo mi’ nilikuwa na crew yangu iliyokuwa inaitwa Bootcamp (Chindo, Dony na Rober). JCB alikuwa na crew yake Hardcore Unit (JCB, Spark Dog, Lord Eyez). Baadae, Watengwa ikawa JCB, Umbwa, Kwele, Dony, Yuzzo, Ghetto Queen (Emmy) na Dwee. Spark alianzisha KCK, na Lord Eyez akaanzisha Nako 2 Nako.
4. Nitakuwa nimekosea nikisema Watengwa mlikuwa underground kwa muda mrefu kabla ya kuanza kusikika kwenye vituo vya redio Tanzania nzima?
Sisi ni underground na milele tutakuwa underground… straight from the Suwer!
5. Ukiacha solo projects mbalimbali, Watengwa — kama kundi — mnakuja na projects nyingine zozote zile?
Kwa sasa watengwa tunajipanga kuleta album ya crew nzima kwa pamoja kama soldiers. Haraka kadri tutakavyoweza!
6. Turudi kwenye projects zako. Kwanini uliamua kuiita album yako “The Future”? Nini hasa malengo yako; wakati una nyimbo mbalimbali kuhusu maisha, mitaa, Hip Hop, maendeleo na siasa?
Album yangu inaitwa The Future kwa sababu nimeona haya maisha na mambo ninayoongelea yapo kwenye nyimbo zangu za kitambo sana, kama vile “Nawaza”. Cha kushangaza ndio maisha ninayoishi sasa hivi.
Wakati huo huo The Future ni future album. Nadhani wengi hawataielewa hadi baadae sana…
7. Hivi, ile hadithi ya “Doggy Danger” ni kweli au?
Hadithi ya Doggy danger ni true story kaka. Sipigi story za uongo kwenye nyimbo zangu… Hip Hop is all about reality.
8. Umezungumza vitu vya msingi sana kwenye wimbo “Usilete Chuki”, baadhi havijadiliwi kabisa kwenye jamii zetu. Kwa mfano, adhabu ya kuchapa watoto mashuleni na nyumbani, athari za migogoro kati ya kina baba na kina mama kwa watoto n.k. Nini hasa kilikusukuma kuandika ule wimbo?
Suala zima la malezi ya watoto bado halijapewa kipaumbele kikubwa kabisa kwenye bara letu la Afrika. Sisemi kuwa tunalelewa vibaya, hapana… ila kuna uonevu mwingi sana na haki za watoto hazitiliwi maanani. Kuchapa sio kufundisha, kwa kifupi…
Inaathiri malezi ya mtoto na matokeo yake anakua kwa uoga sana, na kuathiri maisha yake baadae. Kama unavyojua, kuwa muoga maishani ni sumu. Watoto wa Afrika hawana confidence, hawajiamini kabisa na ni kitu kibaya sana maishani.
9. Suala la usambazaji na mauzo; kuna faida zozote za kuuza album yako kwa njia ya mtandao? Na umejaribu kuisambaza Tanzania? Umeridhika na mauzo?
Kuhusu kuuza album yangu online, kwa kweli nimeridhika sana na nadhani ndo njia sahihi kwa kudhibiti wanyonyaji wa kazi zetu. Kwa upande wa Tanzania nimeisambaza sehemu chache sana. Kama inavyoitwa The Future, sio lazima kuiuza sasa. Ujumbe ulioko ndani hata miaka kumi ijayo nitaiuza bro.
10. Tutegemee album nyingine kutoka kwako — kama Chindo?
Kuhusu album nyingine kwa sasa, tusubiri kidogo. Nataka Watengwa wote tuje kwa pamoja kwanza.
11. Kama mmoja wa watu ambao mmeiona Hip Hop ya Tanzania ikikua, unadhani itakuwa wapi baada ya miaka mitano hivi? Na unawashauri nini chipukizi?
Baada ya miaka mitano nadhani tutakuwa mbali kama tutapeana ushirikiano na kudhibiti wanyonyaji. Wale Wahindi wanaosambaza muziki wafungiwe na serikali ili wasanii wawe na hela, na maendeleo ya sanaa yaonekane.
12. Top 6 MCs wako kutoka Bongo…
1. Hashim Dogo, 2. JCB, 3. Nabii Koko aka Kala Pina, 4. Salu T, 5. Spark Dog (KCK) na 6. Imam Abbas.
Asante sana kwa kunipa nafasi hii!
Shukrani sana Chindo kwa kutumia muda wako kutueleza mambo lukuki kuhusu Watengwa na shughuli zako za kimuziki. Tunawatakia kila la heri wakati mnajipanga kutuletea album nyingine!
Daah mwamba namuelewaga sana huyu
ReplyDelete