facebook

Friday, July 19, 2013

MWANA HARAKATI CHINDO KUTOKA UTENGWANI!

Ni emcee ambaye anaheshimika. Ametoka mbali na anafikiria mbali. Wale ambao wamepata nafasi ya kumsikiliza vizuri wanajua naongelea nini.
Album yake “The Future” ni ya kipekee. Sio kwa sababu ina nyimbo kibao, bali ina nyimbo nyingi na za kutosha za maana. Anahakikisha anawasilisha kitu makini kwenye kila verse.  Wimbo wa kwanza kuanza kusikika hewani kama single ulikuwa “Nakwenda”:
Kuna wimbo mwingine ambao una ladha tofauti kidogo “Tik Tak”:
Tulipata nafasi ya kumuuliza mambo mbalimbali kuhusu yeye binafsi na kundi au familia ya Watengwa, na mahojiano yalikuwa kama ifuatavyo:
1. Chindo, Umbwa Mzee, au Lutuno kutoka Utengwani au Watengwa, hebu tupe tafsiri ya majina yako kwa kifupi…
Kwanza, nashkuru sana mtu mzima kwa kunipa nafasi hii ya kipekee kuongelea suala muhimu sana maishani mwangu!
Nianze na tafsiri ya majina yangu kama ulivyouliza. Chindo ni jina la mtaa tokea mdogo wakati tukicheza michezo ya kujificha (picaboo), ambalo wenzangu kitaani walinibatiza. Umbwa Mzee ni jina la muziki… nilijiita hivyo kama wasanii wengine. Mara nyingi wanamuziki hawatumii majina yao halisi… ni mara chache sana. Lotuno ni jina la ukoo wangu. Mimi naitwa Lomayani Lotuno. Ni jina la Kimasai kwa kuwa mimi ni Mmasai asilia. Linamaana “m’batizwaji”… kidini zaidi!
2. Umeshuhudia gemu ya Hip Hop Tanzania, hasa Arusha, tokea inaanza hadi sasa hivi. Wewe umeingia kwenye gemu lini hasa na nini kilikusukuma uanze kufanya Hip Hop?
Mimi niliingia kenye game rasmi mwaka 1997 nilivyoanza masomo ya sekondari, Namanga secondary school. Kabla ya hapo nilikuwa nasikiliza sana nyimbo za kina MC Hammer, Kool Moe Dee, Busy Bee, Public Enemy, Snoop na Dre, NWA, Warren G, Salt n Pepa, Heavy D na wengine wengi.
Kaka yangu alikuwa mtu wa old skool sana, na alikuwa ananunua tapes nyingi sana na tulikuwa na santuri kibao nyumbani. Kwa kifupi tu, nilikulia katika mazingira ya Hip Hop kwa ujumla. Nakumbuka kaka alikuwa ananinyoa kama kama MC Hammer. Mi’ sikujua kinachoendelea… nilikuwa naona kaka mtu poa sana! Kadri muda ulivyokuwa unaenda ile spirit ilikuwa inajijenga damuni mdo mdo.
3. Ilikuwaje ukaingia kwenye familia kubwa ya Watengwa? Tupe undani wa familia yenu. 
Familia ya Watengwa ilianzishwa mwaka 2002. Baada ya kumaliza masomo ya computer programming Aptech, niliamua kuanzisha studio ili nisihangaike kwenda Dar kurekodi, kwa kuwa kipindi hicho Arusha kulikuwa hakuna studio. Mimi na JCB tuliamua kuungana na kuanzisha chama ‘Watengwa’… kikundi na studio yake.
Kabla ya hapo mi’ nilikuwa na crew yangu iliyokuwa inaitwa Bootcamp (Chindo, Dony na Rober). JCB alikuwa na crew yake Hardcore Unit (JCB, Spark Dog, Lord Eyez). Baadae,  Watengwa ikawa JCB, Umbwa, Kwele, Dony, Yuzzo, Ghetto Queen (Emmy) na Dwee. Spark alianzisha KCK, na Lord Eyez akaanzisha Nako 2 Nako.
4. Nitakuwa nimekosea nikisema Watengwa mlikuwa underground kwa muda mrefu kabla ya kuanza kusikika kwenye vituo vya redio Tanzania nzima?
Sisi ni underground na milele tutakuwa underground… straight from the Suwer!
5. Ukiacha solo projects mbalimbali, Watengwa — kama kundi — mnakuja na projects nyingine zozote zile?
Kwa sasa watengwa tunajipanga kuleta album ya crew nzima kwa pamoja kama soldiers. Haraka kadri tutakavyoweza!
6. Turudi kwenye projects zako. Kwanini uliamua kuiita album yako “The Future”? Nini hasa malengo yako; wakati una nyimbo mbalimbali kuhusu maisha, mitaa, Hip Hop, maendeleo na siasa? 
Album yangu inaitwa The Future kwa sababu nimeona haya maisha na mambo ninayoongelea yapo kwenye nyimbo zangu za kitambo sana, kama vile “Nawaza”. Cha kushangaza ndio maisha ninayoishi sasa hivi.
Wakati huo huo The Future ni future album. Nadhani wengi hawataielewa hadi baadae sana…
7.  Hivi, ile hadithi ya “Doggy Danger” ni kweli au? 
Hadithi ya Doggy danger ni true story kaka. Sipigi story za uongo kwenye nyimbo zangu… Hip Hop is all about reality.
8. Umezungumza vitu vya msingi sana kwenye wimbo “Usilete Chuki”, baadhi havijadiliwi kabisa kwenye jamii zetu. Kwa mfano, adhabu ya kuchapa watoto mashuleni na nyumbani, athari za migogoro kati ya kina baba na kina mama kwa watoto n.k. Nini hasa kilikusukuma kuandika ule wimbo?
Suala zima la malezi ya watoto bado halijapewa kipaumbele kikubwa kabisa kwenye bara letu la Afrika. Sisemi kuwa tunalelewa vibaya, hapana… ila kuna uonevu mwingi sana na haki za watoto hazitiliwi maanani. Kuchapa sio kufundisha, kwa kifupi…
Inaathiri malezi ya mtoto na matokeo yake anakua kwa uoga sana, na kuathiri maisha yake baadae. Kama unavyojua, kuwa muoga maishani ni sumu. Watoto wa Afrika hawana confidence, hawajiamini kabisa na ni kitu kibaya sana maishani.
9. Suala la usambazaji na mauzo; kuna faida zozote za kuuza album yako kwa njia ya mtandao? Na umejaribu kuisambaza Tanzania? Umeridhika na mauzo? 
Kuhusu kuuza album yangu online, kwa kweli nimeridhika sana na nadhani ndo njia sahihi kwa kudhibiti wanyonyaji wa kazi zetu. Kwa upande wa Tanzania nimeisambaza sehemu chache sana. Kama inavyoitwa The Future, sio lazima kuiuza sasa. Ujumbe ulioko ndani hata miaka kumi ijayo nitaiuza bro.
10. Tutegemee album nyingine kutoka kwako — kama Chindo? 
Kuhusu album nyingine kwa sasa, tusubiri kidogo. Nataka Watengwa wote tuje kwa pamoja kwanza.
11. Kama mmoja wa watu ambao mmeiona Hip Hop ya Tanzania ikikua, unadhani itakuwa wapi baada ya miaka mitano hivi? Na unawashauri nini chipukizi? 
Baada ya miaka mitano nadhani tutakuwa mbali kama tutapeana ushirikiano na kudhibiti wanyonyaji. Wale Wahindi wanaosambaza muziki wafungiwe na serikali ili wasanii wawe na hela, na maendeleo ya sanaa yaonekane.
12. Top 6 MCs wako kutoka Bongo…
1. Hashim Dogo, 2. JCB, 3.  Nabii Koko aka Kala Pina, 4. Salu T, 5. Spark Dog (KCK) na 6. Imam Abbas.
Asante sana kwa kunipa nafasi hii!

Shukrani sana Chindo kwa kutumia muda wako kutueleza mambo lukuki kuhusu Watengwa na shughuli zako za kimuziki. Tunawatakia kila la heri wakati mnajipanga kutuletea album nyingine!

MWANA HARAKATI JCB Makalla!


Wasanii wengi waliojengeka na kutengemaa wana sifa nyingi, lakini mara nyingi kila msanii ana kitu kimoja ambacho kinamweka kwenye mwanga.
JCB ni mkongwe, na kitu ambacho kinamtambulisha ni uwezo wake wa kuipa mitaa sauti. Ameegemea zaidi kwenye kuhadithia vinavyotokea kwenye mitaa yetu, huku akiongea kama mmoja wetu; wanaoishi au wale waliopitia maisha ya mitaani.
Ni heshima ya pekee kwa tovuti hii kupata fursa ya kubadilishana mawazo na JCB. Kama kawaida yake, alikuwa na mengi ya kuongelea — kuanzia jinsi alivyoingia kwenye gemu hadi mawazo yake juu ya mwelekeo wa Hip Hop Tanzania.
1. JCB ni nani hasa? Na jina lako ulilipata wapi na linamaanisha nini?
Maana ya JCB ni ‘Jesus Come Black’. Kitambo ilikuwa ‘Jesus Come Back’… mshikaji wangu Spark Doggy ndio alinipa hicho kirefu, lakini mimi nilikuwa bado najiita JCB Black; kipindi hicho kama mwaka 1993 hivi.
JCB limetokana na jina langu Jacob… ukitoa “a” na “o” unapata JCB. Na kutumia “Jesus Come Black” ni kujitambua tu kama mtu mweusi.
2. Ilikuwaje ukaingia kwenye fani ya Hip Hop? Kuna watu waliokupa muongozo au kukuvutia na ukaona na wewe ujaribu?
A-Town ni mji wa Hip Hop toka kitambo, kwa hiyo kuanzia kipindi nakua nilijikuta niko katika mazingira ya Hip Hop. Ndio maana nikavutiwa na Hip Hop. Pia, marehemu kaka yangu, Richard alikuwa ananipeleka disko nilivyokuwa mdogo sana, nilikuwa napenda kucheza break dance.
Kwenye kipindi hicho mara wakatokea watu kama Saleh Jabir, wakaanza kughani kwa Kiswahili. Kwa kweli ilinipa changamoto sana! Watu wengine walionifanya niingie kabisa kwenye Hip Hop ni kama Wagumu Weusi Asilia, Kwanza Unit, Mr II, na watu kama hao.
3. Chindo alitueleza jinsi kundi la Watengwa lilivyoanzishwa, na tungependa wewe utueleze harakati za Hip Hop Arusha. Kuna mwamko wa kipekee wa Hip Hop Arusha, hii inasababishwa na nini?
Mwamko wa Hip Hop Arusha umekuwa mkubwa sana, na ukichukulia watu kibao wanakubali Hip Hop ipo A-Town kwa sasa. Tunajivunia kwa hilo na ninadhani tunatengeneza njia nzuri kwa vizazi vijavyo, kuifanya Hip Hop kuwa ajira kabisa kwa vijana.
4. Kwa upande wa Watengwa, mmekuwa “underground” kwa muda mrefu, ila nadhani heshima mmeipata tokea mwanzoni kabisa. Kujulikana kwenu sasa hivi unadhani kutabadilisha malengo yenu kwenye gemu?
Malengo hayawezi kubadilika kwa sababu muziki iliotuweka hapa ni wa ki-undeground. Sema tunataka kuufanya utupatie maslahi kidogo na kuuboresha kuendana na muda.
5. Aina ya uandishi wako ni adimu, na haujabadilisha msimamo wako! Unawashauri nini wasanii chipukizi?
Kila mtu ana mtindo wake kiuandishi, na muziki pia unahitaji mazoezi. Kwa hiyo kila siku unapokuwa unafanya huo muziki unajikuta unazidi kuboresha mtindo wako. Mi’ nawambia bwana wadogo wanaokuja kwenye game wakomae tukibibwa, mambo yatakuwa poa. Sio mambo ya kuiga style hapa…
6. Hongera kwa kupata tuzo ya Kili kupitia wimbo wako “Ukisikia Paa”, kama wimbo bora wa Hip Hop, ile tuzo wewe unaichukuliaje?
Ile tuzo ilikuwa ni ya wana-Hip hop wote, hususan wa Arusha! Hapo nyuma watu walikuwa hawaamini kama mtaa unaweza kuja kuona tuzo. Kwa kweli ilileta heshima ya Arusha kinoma!
7. Vipi upande wa miradi yako binafsi, unaridhishwa na mapokezi ya albamu yako? Kuna siku ulisema umeshindwa kuelewana na MAMU ili albamu ya pili iingie sokoni. Sasa unajipangaje na mashabiki wako wategemee nini?
Albamu yangu ilipokelewa poa na raia, ila tatizo lilikuwa ni usambazaji arif. Ujue niliiuza mwenyewe mkononi kutokana na mdosi kutaka kunipa fungu dogo sana. Nikaanza kusukuma mzigo mi’ mwenyewe na wana, na tulipata faida mara saba ya mdosi. Lakini tatizo ni kuwa kuna mikoa tulishindwa kufikisha mzigo.
Nakala za Makala Vol 2 imekamilika tayari, ila ndo hivyo bado najipanga tena kuuza mwenyewe Disemba… Bado Serikali haijatutupia jicho.
8. Ukiacha muziki, umekuwa mstari wa mbele kuwasihi vijana wa Arusha kuacha fujo na kupigana/kuchomana visu (beto), hasa baada ya kupoteza mwenzenu hivi karibuni. Mapokezi ya kampeni yenu yalikuwaje?
Hiyo kampeni inaendelea na niko karibu kukutana na wasanii wenzangu wa Arusha kukaa chini na kupiga tamasha moja kabambe. Ila tunataka kuishirikisha na serikali kwa sababu hii ni ishu ya kijamii zaidi. Kabla mwaka haujaisha lazima tamasha hili lifanyike, niko kwenye mikakati za kumuona mbunge wa jimbo langu la Arusha Mjini ili kuomba mawazo yake juu ya hilo tamasha. Ila yuko busy kinoma!
9. Kwa ujumla, unaonaje muelekeo wa Hip Hop Tanzania?
Muelekeo poa sana kwa sisi wasanii wa Hip Hop, tumejaribu kuupaisha muziki huu. Tatizo ni hakuna compuni nzuri inayosimamia kazi za wasanii katika mauzo na vitu kama hivyo. Hatuna haki miliki ya ukweli, mapromota feki kila siku wanaibuka na kuwanyonya wasanii. Serekali ingetutupia jicho kidogo ingekuwa mwake sana. Sema ndio hivyo tunakomaa nao tu. 
10. Tuna freestyles kadhaa za zamani tunazo… mara nyingi Hasheem Dogo, wewe, Chindo na Watengwa wengine, na hata Fid Q, walishiriki. Bado mnafanya yale mambo? Hasheem yuko wapi siku hizi? 
Freestyles zipo zakutosha arif, ujue zamani tulikuwa tunapiga sana freestyles kwa sababu ilikuwa ni mazoezi ya ubongo. Kwa sasa hivi ubongo umeshajengeka vya kutosha, unakuta zile freestyles unazopiga zinakuwa nyimbo sasa.
Kaka Hasheem yuko kitaa lakini ana mambo yake anayafanya tofauti na muziki, ila yuko na tunawasiliana…
11. Kwa kumalizia, tunaomba utupe Top 5 emcees wako kutoka Bongo!
Wa kwanza atakuwa Hasheem Dogo. Jamaa ametupa mbinu sana za kuandika na ku-freestyle. Hasheem is my B.I.G Smallz… nampa heshima kama [ya] Notorious. Wa pili, Jay Moe na Solo Thang, popote hawawezi kuchezea beatkuanzia style na flow; Wateule ni noma. Wa tatu ni Ngosha. Fid Q ni noma…nilimpigia simu niliposikia Neno. Ngosha kiboko yao. Wa nne ni Chindo, ukija katika battles Bongo, hakuna anayeweza kumpiku mwanangu Chindo. N’na-miss kinoma katika muziki huu wa sasa huku TZ. Wa tano ni Lunduno bwana, hawa machalii wataipeleka mbali sana game ya Bongo. Hasa One, namkubali kinoma…
Tunamshukuru JCB kwa kutupa nafasi ya kufanya mahojiano nasi. Tunamtakia kila la heri yeye na wasanii wote kutoka Arusha kwenye harakati zao. Pamoja, inawezekana!

MWANA HARAKATI DAZ NALEDGE KUTOKA KIJENGE JUU!


Kama unafuatilia Hip Hop, hasa upande wa Arusha, utakuwa umesikia kuhusu mradi wa S.U.A. ulioanza shughuli rasmi wiki kadhaa zilizopita. Watengwa wameona kuna umuhimu wa kuwa na jukwaa litakalosaidia kulea na kukuza vipaji vya vijana na kuwawezesha kutimiza ndoto zao kwenye sanaa, bila kusahau kuwaonesha changamoto zinazozunguka jamii zetu.
Mmoja wa watu wanaoendesha mradi huu ni Daz Naledge, mtayarishaji wa muziki wa Hip Hop wa kundi la Watengwa. Na bahati nzuri alitupa fursa ya kufanya mahojiano; kutupa dondoo ya safari yake na mipango ya mradi wa S.U.A.
1. Niambie mzee, vipi ishu pande za Arusha?
Fulu ile laaana arif! Tuko poa, baridi kama kawa, msele kama dawa…[Hahaha!]
2. Kwa wale ambao hawakufahamu vizuri, unajitambulishaje kwao kama mtayarishaji wa muziki wa Hip Hop?
Kama ningeweza ningewapigia beat live, ila kwa wale ambao bado hawamtambui Daz Naledge ningewaomba wapitiemitandao,  pia wachecki hapa ili kusikia kazi nilizofanya hivi karibuni. Nadhani itawapa taswira kamili.
3. Safari yako ya utayarishaji ilianzaje, mpaka ukafika hapa ulipo leo hii?
Waaaaay back nilianza DJ-ing wakati niko shule ya msingi. Mwaka 2005 nilianza kujifunza kutengeneza beats, na ndugu yangu Hamisi Mnaro ndio aliyenifundisha kutumia Fruity Loops. Kipindi hicho nilikuwa nikitoka skonga (siku nyingine nilikuwa natoroka), naenda kwenye internet cafe ya rafiki zangu — big up kwa famillia ya Mshumbushi — nachapa loops taratiiibu. Kusema ukweli nilijifunza mambo mengi kuhusiana na kompyuta.
Prof. Ludigo ndio aliyenifungua akili katika music production. Nilipokutana na Ambross a.k.a Dunga ikawa kama niko chuo kikuu cha muziki.
Mwaka 2010 nikawa producer wa album ya JCB “Nakala za Makalla”. Nikasaidiana na Chindo Man kutengeneza album yake ya Umbwa Mzee The Future. Nikaja kupata nafasi kwenye vyombo vya habari kupitia nyimbo kama Tumetoka Mbali, Sintowasahau Milele, Step Kwa Step, Raff Paper, Drop, Online, n.k.
4. Kuna vitu ambavyo umepitia ambavyo labda ungependa vingekuwa tofauti ili safari yako iwe tofauti kidogo?
Nadhani ni vingi sana. Kuna mambo mengine yasingekuwepo labda ningekuwa mwanasiasa. Ila nachoamini mimi,  kila jambo linatokea kwa sababu. Just be patient with what you are doing.
5. Nadhani kwa upande wa Tanzania, vijana wengi huwa na ndogo za kuwa marapa au MCs na sio utayarishaji wa muziki. Ni kweli, na unawaambia nini wanaotaka kufuata nyayo zako?
Kuupenda muziki ndio sababu kubwa. Mimi nilikuwa naupenda sana, nikawa DJ, ila nikaona haitoshi nikawa naghani. Hata hiyo nikaona haitoshi, nikaamua kuutengeneza [muziki]. Wakati tuko shule kila mtu alikuwa ana ndoto za kuwa daktari ama rubani; mara mtu huyo huyo akiulizwa, siku nyingine anataka kuwa mwalimu mara rais. Ila mimi ilikuwa moja tu: music production.
6. Changamoto gani kubwa unazozipata sasa hivi unapofanya shughuli za utayarishaji?
Changamoto ni nyingi sana, siwezi kutaja zote ila kwa kifupi ni kwamba bado sijapata vyombo vya kisasa vya kuandaa muziki. Halafu bado kuna tatizo la umeme, na mambo ya familia pia… yaani kuna muda inabidi ufanye mambo mengine kwa ajili ya kuendesha maisha ukiacha muziki.
7. Wewe uko kwenye familia kubwa ya Watengwa, ukiacha utayarishaji wa muziki unajishughulisha na shughuli nyingine?
Asilimia kubwa ya maisha yangu nafanya music production. Mara chache huwa nafanya vocal training kwa waimbaji wakati wa mazoezi. Pia nafundisha upcoming producers…
8. Pia, napenda kuchukua nafasi hii kukupongeza kwa kazi uliyoifanya kwenye santuri ya Umbwa Mzee The Future. Ni moja ya albamu nzito kutoka Bongo! Na umechana mule ndani… Bado unachana?
Asante mzee… Sio kila mara ila ikitokea nimepata mzuka nachana ile laana!
9. Tutegemee mikono mingapi kutoka kwako kwenye Ni Full Ile Laana Vol. 2? Au kila kitu kilifanywa Ufaransa? 
Watu wengi tumeshirikiana… Daz Naledge, Chindo, Chapter One Two, DJ PH. Kwa hiyo tusubiri hii kitu kwa kuwa ni kama historia inajirudia, halafu niko ndani… Full Ile Laana!
10. Pia, tumeona mmeandaa kitu kinachoitwa “S.U.A.” Hebu tupe undani kuhusu huu mradi, malengo yake, n.k. Wanaotaka kushiriki wanapaswa kufuata hatua gani?
S.U.A. (Saving Underground Artists) ni jukwaa huru kwa ajili ya vijana kukutana na kubadilishana mawazo kwa kutumia nguzo za Hip Hop. Wahusika hasa ni wasanii chipukizi ambao hawana uwezo wa pesa kufanya sanaa. Lengo kubwa hasa ni kuwalinda vijana chipukizi wenye vipaji, wakati huo huo kutumia jukwaa kuelimisha jamii. Kutakuwa na vitu kama semina kwa ajili ya wasanii — kuwafundisha ili waje kuwa wasanii wazuri na kuwaelemisha kuhusu sehemu na majukumu yao kwenye jamii.
S.U.A. kutakuwa  na kipindi cha “edu-tain”, kulingana na maudhui ya siku husika, kwa mfano malaria. Kutakuwa na mtu mwenye ufahamu au ujuzi ataongelea jambo husika kwa kina. Ukiacha yote hayo, kutakuwa na mashindano ya freestlyling, cypher, grafiti, n.k. Kwa maelezo zaidi tunaomba watu watembelee ukurasa wetu wa S.U.A.
11. Wewe binafsi unataka “S.U.A.” iwe wapi baada ya miaka mitatu hivi, na mnafanya nini kuhakikisha mnafikia malengo yenu?
Miaka mitatu tunategemea tuwe tumefika kona zote za Afrika Mashariki. Ili kufanikisha malengo yetu tumeanza na Kijenge, na mwisho wa mwaka tunategemea kufunga msimu huu wa kwanza wa S.U.A. uliopewa jina la “The Preparation”.
Mwakani tutaanza kwenda kona zote za Arusha, mtaa kwa mtaa, halafu tutaenda mikoa mingine kabla ya kuvuka mipaka. Nashukuru niko na timu ya watu waliojitolea kwa moyo kufanikisha hii MOVEMENT. Pia tunakaribisha wote wenye uwezo wa kudhamini, wasisite kuwasiliana na S.U.A.
12. Kwa kumalizia, tupe Top 5 emcees  na 2 Top producers kutoka Bongo! 
Watengwa, One the Incredible, Joh Makini , Fid Q na Jay Moe. Kwa upande wa watayarishaji, P. Funk Majani na Ambross a.k.a Dunga.
Shukrani sana Daz kwa kutupa undani wa shughuli na miradi anayoratibu na akishirikiana na kikosi kizima cha Watengwa. Ni matumaini yetu matunda ya juhudi zao yataanza kuonekana, na tunawatakia kila la heri!

Thursday, July 18, 2013

MWANA HARAKATI MZEE Nelson Mandela afikisha miaka 95!

Leo ni siku ya kimataifa ya shujaa wa kupinga Ubaguzi wa Rangi Afrika Kusini, Nelson Mandela.
Rais mstaafu wa Afrika Kusini Nelson Mandela pia anaadhimisha siku ya kuzaliwa leo akitimiza miaka 95 akiwa bado amelazwa hospitalini.

Serikali ya Afrika Kusini imewaomba wananchi wake kusaidia watu wasiojiweza na kutenda mema kama heshima kwa Madiba.Mandela amelazwa hospitalini kutokana na matatizo ya kupumua.
Rais Barack Obama alimtakia kila la heri Mandela anayetambulika kama shujaa wa vita dhidi ya ubaguzi wa rangi.
Madiba anasalia hospitalini mjini Pretoria, lakini madaktari wake wamethibitisha kuwa afya yake inaendelea kuimarika.
Naye rais Jacob Zuma amemtakia kila la heri Mandela katika sherehe za siku ya kuzaliwa kwake.
Watoto kwenye shule kote nchini humo walitarajiwa kuanzisha sherehe hizo kwa kumuimbia Mandela wimbo wa kusherehekea siku ya kuzaliwa kwake katika siku ambayo pia iliadhimishwa miaka kumi na mitano ya ndoa yake kwa mke wake wa tatu Graca Machel.
Mwanawe Mandela wa kike, Zindzi, alisema Jumatano kuwa afya ya Mandela imeimarika pakubwa na kwamba alimpata akiwa anatazama televisheni huku akiwasiliana kwa macho yake na mikono alipomzuru wiki jana.
''Nina matumaini kuwa atarejea nyumbani wakati wowote sasa'' Zinzi aliambia shirika la habari la Uingereza Sky News.
Siku ya kimataifa ya Mandela iliwekwa na umoja wa mataifa kama njia ya kumkumbuka mshindi huyo wa tuzo ya amani ya Nobel kwa juhudi zake za kupatanisha watu.
Mandela anasifika kote duniani kwa juhudi zake za kumaliza vita vya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini. Baadaye alichaguliwa kama rais wa kwanza mwafrika wa nchi hiyo mwaka 1994.

Chama cha kitaifa cha (ANC) kimesema kuwa katika siku hii ya kusherehekea siki ya kimataifa ya Mandela, ni heshima kwa miaka yake 95 kwa maisha yake aliyoishi vyema na ambayo ameitumia kupigania wananchi wa Afrika Kusini.

Thursday, July 11, 2013

MWANA HARAKATI ROMA AKICHEZA BASKET BALL!

 
 
 
 
 
Huyu hapa roma mkatoliki akifanya yake kwenye mchezo wa kikapu.

Wednesday, July 10, 2013

PROFESSOR JAY AFIWA NA MAMA YAKE MZAZI!


Kwa Mujibu Wa Gardner G Habash aliye kuwa karibu na rapper Profesa Jay, Leo Jioni Walipata taarifa kuwa mama yake mzazi amepata ajali na yupo kituo cha polisi akichukua PF3 ili akapate matibabu. Baada ya Profesa kupokea simu, palianza kuwa na tatizo la mawasiliano, Profesa alimpigia simu Mama yake mzazi na ndipo alipo mwambia Profesa kuwa ni kweli amepata ajali na anakwenda hospitalini. 

Katikati ya ule muda aliotumia Profesa Kufika Hospitalini, Mama Yake Mzazi Bi Rosemary Majanjara Alifariki Dunia. Pole kwa Familia Ya Profesa Jay, Ndugu na Marafiki Zao.

Pole sana Profesa Jay kwa kuondokewa na Mama yako kipenzi. Mungu akutie nguvu katika kipindi hiki kigumu.

Saturday, July 6, 2013

MWANA HARAKATI WAKAZI HAPATA SHAVU LA KUFANYA SHOW KATIKA JUMBA LA BIG BROTHER JUMAPILI HII!


Wakazi ni Msanii anaye fanya muziki wa hip hop Hapata shavu la kufanya show katika jumba la big brother Africa!