facebook

Friday, July 19, 2013

MWANA HARAKATI DAZ NALEDGE KUTOKA KIJENGE JUU!


Kama unafuatilia Hip Hop, hasa upande wa Arusha, utakuwa umesikia kuhusu mradi wa S.U.A. ulioanza shughuli rasmi wiki kadhaa zilizopita. Watengwa wameona kuna umuhimu wa kuwa na jukwaa litakalosaidia kulea na kukuza vipaji vya vijana na kuwawezesha kutimiza ndoto zao kwenye sanaa, bila kusahau kuwaonesha changamoto zinazozunguka jamii zetu.
Mmoja wa watu wanaoendesha mradi huu ni Daz Naledge, mtayarishaji wa muziki wa Hip Hop wa kundi la Watengwa. Na bahati nzuri alitupa fursa ya kufanya mahojiano; kutupa dondoo ya safari yake na mipango ya mradi wa S.U.A.
1. Niambie mzee, vipi ishu pande za Arusha?
Fulu ile laaana arif! Tuko poa, baridi kama kawa, msele kama dawa…[Hahaha!]
2. Kwa wale ambao hawakufahamu vizuri, unajitambulishaje kwao kama mtayarishaji wa muziki wa Hip Hop?
Kama ningeweza ningewapigia beat live, ila kwa wale ambao bado hawamtambui Daz Naledge ningewaomba wapitiemitandao,  pia wachecki hapa ili kusikia kazi nilizofanya hivi karibuni. Nadhani itawapa taswira kamili.
3. Safari yako ya utayarishaji ilianzaje, mpaka ukafika hapa ulipo leo hii?
Waaaaay back nilianza DJ-ing wakati niko shule ya msingi. Mwaka 2005 nilianza kujifunza kutengeneza beats, na ndugu yangu Hamisi Mnaro ndio aliyenifundisha kutumia Fruity Loops. Kipindi hicho nilikuwa nikitoka skonga (siku nyingine nilikuwa natoroka), naenda kwenye internet cafe ya rafiki zangu — big up kwa famillia ya Mshumbushi — nachapa loops taratiiibu. Kusema ukweli nilijifunza mambo mengi kuhusiana na kompyuta.
Prof. Ludigo ndio aliyenifungua akili katika music production. Nilipokutana na Ambross a.k.a Dunga ikawa kama niko chuo kikuu cha muziki.
Mwaka 2010 nikawa producer wa album ya JCB “Nakala za Makalla”. Nikasaidiana na Chindo Man kutengeneza album yake ya Umbwa Mzee The Future. Nikaja kupata nafasi kwenye vyombo vya habari kupitia nyimbo kama Tumetoka Mbali, Sintowasahau Milele, Step Kwa Step, Raff Paper, Drop, Online, n.k.
4. Kuna vitu ambavyo umepitia ambavyo labda ungependa vingekuwa tofauti ili safari yako iwe tofauti kidogo?
Nadhani ni vingi sana. Kuna mambo mengine yasingekuwepo labda ningekuwa mwanasiasa. Ila nachoamini mimi,  kila jambo linatokea kwa sababu. Just be patient with what you are doing.
5. Nadhani kwa upande wa Tanzania, vijana wengi huwa na ndogo za kuwa marapa au MCs na sio utayarishaji wa muziki. Ni kweli, na unawaambia nini wanaotaka kufuata nyayo zako?
Kuupenda muziki ndio sababu kubwa. Mimi nilikuwa naupenda sana, nikawa DJ, ila nikaona haitoshi nikawa naghani. Hata hiyo nikaona haitoshi, nikaamua kuutengeneza [muziki]. Wakati tuko shule kila mtu alikuwa ana ndoto za kuwa daktari ama rubani; mara mtu huyo huyo akiulizwa, siku nyingine anataka kuwa mwalimu mara rais. Ila mimi ilikuwa moja tu: music production.
6. Changamoto gani kubwa unazozipata sasa hivi unapofanya shughuli za utayarishaji?
Changamoto ni nyingi sana, siwezi kutaja zote ila kwa kifupi ni kwamba bado sijapata vyombo vya kisasa vya kuandaa muziki. Halafu bado kuna tatizo la umeme, na mambo ya familia pia… yaani kuna muda inabidi ufanye mambo mengine kwa ajili ya kuendesha maisha ukiacha muziki.
7. Wewe uko kwenye familia kubwa ya Watengwa, ukiacha utayarishaji wa muziki unajishughulisha na shughuli nyingine?
Asilimia kubwa ya maisha yangu nafanya music production. Mara chache huwa nafanya vocal training kwa waimbaji wakati wa mazoezi. Pia nafundisha upcoming producers…
8. Pia, napenda kuchukua nafasi hii kukupongeza kwa kazi uliyoifanya kwenye santuri ya Umbwa Mzee The Future. Ni moja ya albamu nzito kutoka Bongo! Na umechana mule ndani… Bado unachana?
Asante mzee… Sio kila mara ila ikitokea nimepata mzuka nachana ile laana!
9. Tutegemee mikono mingapi kutoka kwako kwenye Ni Full Ile Laana Vol. 2? Au kila kitu kilifanywa Ufaransa? 
Watu wengi tumeshirikiana… Daz Naledge, Chindo, Chapter One Two, DJ PH. Kwa hiyo tusubiri hii kitu kwa kuwa ni kama historia inajirudia, halafu niko ndani… Full Ile Laana!
10. Pia, tumeona mmeandaa kitu kinachoitwa “S.U.A.” Hebu tupe undani kuhusu huu mradi, malengo yake, n.k. Wanaotaka kushiriki wanapaswa kufuata hatua gani?
S.U.A. (Saving Underground Artists) ni jukwaa huru kwa ajili ya vijana kukutana na kubadilishana mawazo kwa kutumia nguzo za Hip Hop. Wahusika hasa ni wasanii chipukizi ambao hawana uwezo wa pesa kufanya sanaa. Lengo kubwa hasa ni kuwalinda vijana chipukizi wenye vipaji, wakati huo huo kutumia jukwaa kuelimisha jamii. Kutakuwa na vitu kama semina kwa ajili ya wasanii — kuwafundisha ili waje kuwa wasanii wazuri na kuwaelemisha kuhusu sehemu na majukumu yao kwenye jamii.
S.U.A. kutakuwa  na kipindi cha “edu-tain”, kulingana na maudhui ya siku husika, kwa mfano malaria. Kutakuwa na mtu mwenye ufahamu au ujuzi ataongelea jambo husika kwa kina. Ukiacha yote hayo, kutakuwa na mashindano ya freestlyling, cypher, grafiti, n.k. Kwa maelezo zaidi tunaomba watu watembelee ukurasa wetu wa S.U.A.
11. Wewe binafsi unataka “S.U.A.” iwe wapi baada ya miaka mitatu hivi, na mnafanya nini kuhakikisha mnafikia malengo yenu?
Miaka mitatu tunategemea tuwe tumefika kona zote za Afrika Mashariki. Ili kufanikisha malengo yetu tumeanza na Kijenge, na mwisho wa mwaka tunategemea kufunga msimu huu wa kwanza wa S.U.A. uliopewa jina la “The Preparation”.
Mwakani tutaanza kwenda kona zote za Arusha, mtaa kwa mtaa, halafu tutaenda mikoa mingine kabla ya kuvuka mipaka. Nashukuru niko na timu ya watu waliojitolea kwa moyo kufanikisha hii MOVEMENT. Pia tunakaribisha wote wenye uwezo wa kudhamini, wasisite kuwasiliana na S.U.A.
12. Kwa kumalizia, tupe Top 5 emcees  na 2 Top producers kutoka Bongo! 
Watengwa, One the Incredible, Joh Makini , Fid Q na Jay Moe. Kwa upande wa watayarishaji, P. Funk Majani na Ambross a.k.a Dunga.
Shukrani sana Daz kwa kutupa undani wa shughuli na miradi anayoratibu na akishirikiana na kikosi kizima cha Watengwa. Ni matumaini yetu matunda ya juhudi zao yataanza kuonekana, na tunawatakia kila la heri!

No comments:

Post a Comment