NI MAPEMA SANA KALA PINA!!!!
Kalama Masoud Suleiman ndio jina halisi la mtu ambaye anafahamika kama Kala Pina, Nabii Koko, Kamanda Mura, Mbunge Mtarajiwa n.k. Licha ya Kalama Masoud kuwa na ‘a.k.a’ nyingi ni ‘a.k.a’ moja tu ambalo inatambulika zaidi ambayo ni Kala Pina. Kwa mujibu wa maelezo yake mwenyewe anasema “maana ya Pina ni kitu kipya.. kwa hiyo Pina anakuwa mpya kila siku, hawezi kuwa yule yule wa zamani” (clouds, 2015).
Kabla ya kuzama katika ulingo wa siasa za vyama, Kala Pina amekuwa katika sanaa ya muziki akijikita katika mapambano ya kuisimamisha Hip Hop nchini Tanzania. Hakuna rekodi za uhakika ambazo zinaonesha ni lini hasa Kala Pina alianza kufanya muziki ila kuna uwezekano akawa ameanza baada ule wakati ambao Chid Benz aliousema kwamba “alianza muziki Hashim bado anachana… Profesa mwembamba… Kala Pina anauza flana” katika wimbo ambao ameshirikishwa na Ay na Mwana FA.
Kauli hiyo inaweza kuwa sababu iliyochochea pia kutokuelewana kwa Kala Pina na Chid Benz kiasi cha Chid Benz kupokea ‘nakozi’ miaka ya hivi karibuni kutoka kwa pina. Kwa ujumla Kala Pina ni msanii ambaye sanaa yake zinapambwa na ubabe/nguvu kama mbinu ya ukombozi ambao unasadifu kabisa jina la kundi lake, Kikosi Cha Mizinga chenye maskani yake Kinondoni Block 41. Kwa hivyo kutofautiana na Kala Pina muda mwingine ni kama “Kujitoa mhanga zaidi ya yesu msalabani” kama yeye mwenyewe alivyosema kwenye ‘Umoja ni Nguvu’ huwezi kitakupata nini ukithubutu kukutwa.
Katikati mwa Miaka ya 2000 kuelekea mwishoni ambapo marapa wengi walipoanza kufanya nyimbo za siasa zikiitaja moja kwa moja serikali ama majina ya viongozi wake. Kwa wengi kilionekana ni kitu kipya lakini Kala Pina aliwahi kukaririwa akisema katika mahojiano na kituo kimoja cha redio akisema kwamba yeye alichana waziwazi viongozi wa serikali miaka mingi iliyopita katika kibao cha ‘Tunasonga’ aliposema kwamba yuko “Tayari kukipaka hata mbele ya bwana mkapa”.
Kala Pina sio rapa wa kwanza ambaye aliweza kuwachana viongozi moja kwa moja katika nyimbo ikumbukwe katika makala moja hivi, zavara (2012) aliwahi kusema kuwa mwishoni mwa miaka ya 80 (kama sio 88) msanii aitwaye Dika Shap aliwahi kufanya wimbo ambao alimuimba Raisi wa wakati huo Ndugu Ali Hassani Mwinyi. Tofauti ya miaka inamfanya Dika Shap awe mchanaji wa mwanzo mwanzo kumchana kiongozi wa juu wa serikali.
Baada ya kuchana katika muziki mambo ya siasa, katika uchaguzi wa Mwaka 2010 Kala Pina aliamua kujitosa katika majukwaa siasa kugombea udiwani kupitia chama cha wananchi CUF. Katika uchaguzi huo Pina alishindwa kwa sababu anayoieleza kwamba “lililopofika zoezi la kuhesabu kura ghafla aliingiwa na kitu jichoni na kupata maumivu makali mno na kukimbilia nyumbani watu walipomuangalia hawakuona kitu na baada ya kufanya dua alipata nafuu na kurudi kituo cha kupigia kura, akakukuta mambo yameshaharibika” (Ayo, 2015).
Pina anasema jicho hilo lilimuuma kwa sababu za kishirikina (yeye akiziita sababu za kimila na kitamaduni). Katika mahojiano aliwahi kuulizwa kama ni kweli siasa inahusishwa sana na imani za kishirikina akajibu “hayo ni mambo ya mila na utamaduni yapo dunia nzima.. tena kwenye siasa yana nafasi kubwa sana kwa sababu ni masuala ya utawala”. Alipoulizwa kwamba kama yeye (Pina) anaye mganga wake alikwepa kujibu swali hilo lakini katika uchaguzi wa 2015 alisema atajipanga kwa mitindo yote ya kisayansi, kiutamaduni, kiuchumi n.k kutokana na kuingia kichwa kichwa kwenye uchaguzi wa 2010 (Clouds, 2015).
Baada ya kushindwa mara ya kwanza, Kala Pina alisema kwamba atajipanga kiutamaduni, kiuchumi, kisayansi n.k lakini nafikiri hakujipanga kikamilifu kutokana na kushindwa tena katika uchaguzi wa 2015 na safari hii akigombea ubunge wa Kinondoni. Safari hii pia aligombea kupitia chama kipya cha ACT. Sababu ya kuhama CUF kwenda ACT wakati alishiriki michakato yote kutafuta mgombea atakayesimamishwa kugombea ubunge jimbo la Kinondoni hazifahamiki. Sijui ni nini kilitokea, labda jina lake ‘lilikatwa’ katika mchakato wa kutafuta mgombea akaona atimkie ACT au hakupenda Lowassa kujiunga na UKAWA akaamua kung’atuka.
Ikumbukwe niliwahi kuandika kwamba “Kala Pina alishindwa kupiga hesabu zake vizuri kwa sababu chama alichokihama (CUF) na kwenda ACT ndicho kilichoshinda uchaguzi. Kwa lugha ya mtaani tunasema alichengana au alipishana na gari la mshahara” (Hanzi, 2015). Nilimtazama katika Luninga baada ya matokeo kutangazwa alihojiwa akasema anapinga matokeo hayo na amekataa kusaini kutokana uwepo wa mapungufu hususani zoezi la kuhesabu kura.
Licha ya Mapungufu katika mchakato wa uchaguzi aliyoyaeleza nafikiri sababu ya kushindwa ambayo ingemfaa zaidi Kala Pina ni ile aliyosema Afande Sele kwamba “watu wengi hawakuwa wanakifahamu chama alichokuwa akigombea” (Ayo, 2015) ambacho ni ACT alichomo Kala Pina kutokana na uchanga wake katika medani ya siasa. Pia niliwahi kusikitika jinsi ulivyojibu swali uliloulizwa kwamba ungekuwa ndani ya bunge wakati wa sakata la escrow ungefanyaje ukajibu kwamba ungetoa kichapo bungeni kwa sababu ya kinga ya wabunge. Nadhani pia wananchi waliangalia pia uwezo wa kujenga hoja na kupangua hoja.
Baada ya uchaguzi wa udiwani, ubunge na uraisi kuisha na Dkt John Pombe Maghufuli kutangazwa na kuapishwa kuwa Raisi wa Tanzania Kala Pina ameibuka na kitu kipya tena kama ambavyo jina lake lilivyo. Hivi karibuni ametoa wimbo ambao umelenga kusifia utendaji kazi wa raisi Dkt Magufuli ambaye toka aapishwe hajatimiza hata miezi mitatu. Nakiri kwamba ni kitu kizuri ambacho kinaweza kumtia morali ya kazi mheshimiwa kuendelea kuwatumikia watanzania kwa “kiwango cha lami” lakini waswahili hawakukosea pia kusema “Mgema akisifiwa, Tembo hulitia maji”.
Kwenye huu wimbo Kala Pina licha ya kumsifia sana Dkt Magufuli lakini kuna sehemu anasema anaona kama Miujiza kwa vitu vinavyoendelea. Hatua ambazo anazozichukua magufuli ni nzuri japo ni robo ya robo ya robo ya hatua ambazo zinapaswa kuchukuliwa. Miujiza ni magufuli kutenda kile ambacho wapinzani walitaka kufanya. Ila miujiza mingine ni pale Kala Pina ambaye ni mpinzani wa chama tawala anaposema “wapinzani wamefungwa kufuli wamekosa cha kusema”. Najiuliza tu Kala Pina yuko chama cha upinzani au yuko chama tawala. Kama yuko Upinzani kwanini asiseme “wapinzani tumefungwa kufuli” na yeye akajijumuisha.
Kala pina anasema miaka yote ambayo amefanya muziki hajawahi “kumsifia mtawala lakini kwa magufuli hilo halina mjadala” uzalendo umemshinda. Kala Pina anamchukulia maghufuli kama mzalendo ambaye hajatokea miaka mingi na amekuja kama mkombozi tuliyemngoja miaka kadhaa. Ni jambo zuri kusifia lakini nimkumbushe Kala Pina mambo yafuatayo:-
Mtatiro (2015) alishawahi kusema wanaomkosoa magufuli hawana cha kupoteza ili mradi wanasema ukweli na unapaswa kufanyiwa kazi. Hawa ni watu wanaoiona dunia ya mbele na kuiishi sasa na wanaomtetea magufuli kwa kila kitu hawa watajifunza pindi watakapoifikia dunia ya mbele. Akaendelea kusema “anachofanya magufuli leo kiliongelewa jana na juzi na wakosoaji, waliishi jana na juzi lakini waliiona dunia ya leo”.
Kaka Kala Pina asije kuwadharau wakosoaji wa magufuli kwa sababu “ndiyo chanzo cha mabadiliko duniani, hawa ni watu wanaohoji kila kitu mpaka wanaingia kaburini. Hawa ni watu ambao watapiga kelele kupinga safari za nje, ukizifuta watapiga kelele kuhoji pesa za safari zilizokatwa zimekwenda wapi, hawa ni watu watakaoenda mbali kutaka kuwepo na sharia za kuelekeza safari za nje, na ukiwatungia sharia watakuja mbele kuhoji kama kweli itajenga misingi waliyoipigia kelele, ukishatunga watakuja kukosoa inahitaji marekebisho, ukiifanyia marekebisho watakuhoji mbona huitekelezi ipasavyo, na ukianza kuitekeleza watakuuliza imeleta manufaa gani…” (Ibid).
Nikukumbushe pia Nas Escoba alishawahi kusema “trust no black leaders” akiwa na maana usimwamini kiongozi mweusi. Viongozi weusi wengi wamekuwa vibaraka wa nchi za magharibi. Usisahau kwamba Obama ni mtu mweusi lakini yeye na wenzie ndio waliomuua Ghadafi huku viongozi wote wa nchi za Kiafrika hakuna aliyetoa msaada wowote hata kwa kukemea tu uvamizi huo.
Immortal Technique ni mchanaji ambaye Kala Pina huwa anajilinganisha nae kiitikadi aliwahi kusema “Capitalism and Democracy are not synonymous” kwamba neno “ubepari na demokrasia sio maneno mbadala” ila mabepari huyalandanisha ili kusambaza demokrasia yao. Kimsingi kila nchi inatakiwa kuwa na demokrasia yake ikiwa tu wananchi wenyewe ndio wameamua demokrasia hiyo. Sisi Tanzania tumeshapoteza demokrasia yetu miaka mingi, mambo yetu mengi yanaamuliwa nje.
Kimsingi hizi pongezi kupitia wimbo huu wa Kala Pina zimetoka mapema sana raisi akiwa hajamaliza hata miezi mitatu ofisini. Kilichofanyika ni kama kumpa msanii tuzo ya wimbo bora wakati bado hajaurekodi. ungesubiri 2020 ndipo ungeweza kufanya tathmini yakinifu tofauti na hapo wengine wanaweza kuona kama “sizoni twu ya kampeni”. Mapema yote hii amemsifia vipi huko mbele akabadilika na mambo yakawa ndivyo sivyo… itakuaje? au utawaeleza nini tena watanzania.
Nimalize kwa kunukuu maneno haya yanayosema kwamba “Kiongozi mwerevu hana cha kujifunza kwa waridhikaji, wapongezaji na wakubali kila kitu” (Mtatiro, 2015). Kwa hivyo tuendelee kukosoa kwa kadri inavyowezekana na pia tusifie pale inapobidi lakini kwa umakini na tahadhari ili tusivuke mipaka ya pongezi. Pongezi za Kala Pina zimetoka mapema sana… angesubiri subiri kidogo. Dkt Magufuli ana majipu mengi ya kutumbua na nikikutajia utaona kama bado hajaanza kazi. Heri ya mwaka mpya. Cheers.
Imeandikwa na
Malle Hanzi
O715076444
©2016
No comments:
Post a Comment